www.domdaily14.blogspot.com

Wednesday, 4 January 2017

RC aomba sheria ya kutembea na sime ifutwe

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ameomba serikali kufuta sheria inayoruhusu watu kutembea na silaha kama vile sime, panga, mkuki au mshale mkoani humo.

Amesema hatua hiyo itapunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji mkoani humo.

 Alitoa ombi hilo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba katika mikutano ya hadhara katika vijiji vya Tindiga na Dumila. Kwa upande wake, Nchemba alisema kuanzia jana ikitokea mkulima ama mtu yeyote amejeruhiwa kwa sime, panga, mkuki au mshale mkoani Morogoro, serikali itafuta sheria inayoruhusu watu kutembea na silaha.

Alisema hatua hiyo inatokana na ombi la Mkuu wa Mkoa, Dk Kebwe la kufuta au kurekebisha sheria hiyo ili kupunguza vifo na majeruhi katika migogoro ya wakulima na wafugaji.

 Aidha, waziri huyo ameunda tume itakayokuwa na jukumu la kuwaorodhesha viongozi wa serikali wa ngazi mbalimbali wilayani Kilosa mkoani Morogoro, wanaodaiwa kwenda kinyume na sheria ya utendaji kazi. Majina yao yatawasilishwa ofisini kwake kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria. 

 Alitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti wilayani Kilosa jana, alipozungumza na viongozi wa Serikali ya wilaya hiyo na mkoa, wakiongozwa na Dk Kebwe.

 Aliwaambia wafugaji na wakulima kuwa hakuna sababu yoyote ile, itakayosababisha mtu kuchukua hatua za kumuua binadamu mwezie, kwani uhai haulinganishwi na thamani ya kitu chochote kile. Aliwaonya viongozi wa ngazi mbalimbali, kuacha urafiki na wauaji.

 Alisisitiza kiongozi yoyote atakayebainika kuwa na ushirikiano na muuaji, basi na yeye ataunganishwa kwenye kesi ya mauaji .

 Waziri Nchemba alivitaka vyombo vya dola na vya kisheria, kutosubiri wananchi wachukue sheria mkononi, bali wachukue sheria na adhabu inayostahiki wote wenye kutenda makosa ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa mara moja. 

 “Duniani kote sheria isipochukua mkondo wake kwa wahalifu, basi wananchi watachukua sheria mkononi“ alisema. Aliwataka wafugaji kukutana na kujadili wao wenyewe namna ya kuacha tabia hizo.

No comments:

Post a Comment

Toa Maoni Yako Hapa (Zingatia Maadili)

Blog Archive