KAIMU Mkurugenzi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Tito
Mwinuka ameahidi kuongeza ufanisi wa shirika katika kuzalisha umeme
sambamba na kudhibiti upotevu wa umeme na mapato.
Aidha, amepanga kupambana na wezi wa umeme na vishoka ambao wamekuwa
wakiliibia shirika hilo, jambo ambalo linapunguza mapato ya shirika.
Mwinuka aliyasema hayo kwenye mahojiano, yaliyolenga kuangalia
vipaumbele vyake mara baada ya kukabidhiwa wadhifa wa kuliongoza shirika
hilo.
Mwinuka ambaye alikuwa ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM)
na Mkuu wa Idara ya Mekanika na Uhandisi wa Viwanda Chuo cha Uhandisi
na Teknolojia (CoET) cha UDSM, aliteuliwa kushika wadhaifa huo, baada ya
Rais John Magufuli kutengua uteuzi wa Felchesmi Mramba.
Akitaja baadhi ya vipaumbe vyake, Mwinuka ikiwa ni pamoja na upanuzi wa
uwezo wa shirika wa kuzalisha umeme, lengo likiwa ni kuzalisha umeme wa
ziada, ambao utaweza kuwavutia wawekezaji hususani sekta ya viwanda.
“Sisi zao letu ni umeme, itakuwa vizuri katika miaka mingi inayokuja
tukahakikisha tunakuwa na umeme wa kutosha. Tusipoweza kupanua uwezo wa
kuzalisha umeme, itafika wakati tutashindwa kuongeza kiwanda wala
kumuunganishia mteja yeyote. “Tutakuwa na mikakati ya muda mfupi, kati
na muda mrefu, hili ni suala endelevu.
Ingawa kwa sasa mahitaji na uwezo wa shirika wa kuzalisha umeme
haupishani sana, lengo letu ni kuhakikisha tunakuwa na uwezo wa
kuzalisha ziada wa zaidi ya megawati 600, unaweza kumwambia mwekezaji
unaweza kuzalisha umeme wa ziada." Kuhusu suala la miundombinu, Mwinuka alisema atahakikisha miundombinu
kama mitambo, mabwawa na njia za kusafirishia umeme, zinakuwa na ubora
na uwezo ili kuongeza ufanisi wa huduma.
“Katika miundombinu ambayo tunayo, kwa maana ya mitambo tulionayo ya
kuzalisha umeme, mabwawa na njia za kusafirishia inatakiwa kuwa bora na
yenye uwezo, ili isije ikaporomoka."
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni Yako Hapa (Zingatia Maadili)