www.domdaily14.blogspot.com

Tuesday, 31 January 2017

Haya hapa Matokeo ya Kidato cha Nne na mtihani wa Maarifa 'QT' 2016

Leo January 31 2017 Baraza la mitihani Tanzania ‘NECTA’ limetangaza matokeo ya kidato cha nne ‘CSEE 2016’ na matokeo ya mtihani wa maarifa (QT) 2016
Kwa urahisi unaweza kuyaona matokeo ya kidato cha nne kwenye link hii hapa iliyoandikwa ‘CSEE 2016’ >>>CSEE 2016
Unaweza pia kuyatazama matokeo ya mtihani wa maarifa (QT) 2016  >>>(QT) 2016

Gazeti lapewa saa 24 kumuomba radhi Rais Magufuli

Onyo limetoka kwenye Idara ya habari maelezo kupitia kwa Mkurugenzi wake Dr. Hassan Abbasi ambapo gazeti lililoandika kichwa cha habari ‘UFISADI NDANI YA OFISI YA JPM‘ limepewa saa 24 kuomba radhi.

Taarifa ya Idara hiyo imesema ‘licha ya habari hiyo kujenga dhana kuwa Rais John Pombe Magufuli anahusika na kinachoitwa ufisadi, msingi wa taarifa husika ni tatizo la manunuzi shirika la elimu Kibaha.

Kwa kuwa ni jambo lililodhahiri kuwa shirika la elimu Kibaha sio ofisi, Idara wala kitengo ndani ya Ofisi ya Rais, Mwandishi na Mhariri wa habari husika wamedhihirisha malengo ya kumchafua Rais binafsi kwa jamii.

Serikali inawaagiza Wahariri wa gazeti hilo kujitathmini na kuchukua hatua kwa kutumia kifungu cha 410 cha sheria ya huduma za habari 2016 kinachowapa fursa ya kuomba radhi, kwa kumuomba radhi Rais ndani ya saa 24 kuanzia saa kumi jioni ya January 30 2017.

Iwapo wahusika wataona muhali kufanya hivyo, Serikali itachukua hatua kali kwa mujibu wa sheria na masharti ya usajili wa gazeti husika, Tunaendelea kuwashukuru Wanahabari wanaofuata madili ya taaluma. – Dr. Hassan Abbasi.

Ugomvi wa DC, Mbunge wa CCM wamfikia Waziri Mkuu

Dodoma; Mgogoro baina ya Mbunge wa Chemba (CCM), Juma Nkamia na mkuu wa wilaya hiyo, Saimon Odunga umechukua sura mpya, safari hii ukiibuka katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Dodoma (RCC) ambayo imeamua ufikishwe kwa Waziri Mkuu. Kikao hicho ambacho kilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana kilifanyika katika ukumbi wa Chuo cha Mipango. Baada ya Odunga kupewa nafasi ya kuchangia ajenda mara baada ya Majaliwa kuondoka, aliomba ushirikiano kutoka kwa wabunge ilikutekeleza shughuli za maendeleo. 

“Ninaomba waheshimiwa wabunge watusaidie kulisemea hili kwa sababu hali ni mbaya katika sekta nyingi,” alisema. Akizungumza katika kikao hicho, Nkamia, ambaye aliwahi kuwa naibu waziri, alianza kwa kumuomba Rugimbana kusaidia katika sekta ya ardhi akisema ina matatizo mengi na kutoa mfano wa Wilaya ya Chemba. Alisema katika wilaya hiyo kuna tapeli wa ardhi ambaye amesaidiwa na viongozi kupata ardhi yenye ukubwa wa ekari 500 kinyume na sheria. Alihoji sababu za mkuu huyo wa wilaya kutaka wabunge washiriki katika kusukuma hoja mbalimbali za maendeleo, wakati anadharau wabunge, mwenyekiti wa halmashauri na viongozi wengine wa chama wilayani humo. “Huyu ni mkuu wa wilaya ambaye anaongoza kwa rekodi ya kuwakamata watu kwa kutumia madaraka yake. Nimesikia jana (juzi) kuwa na mimi nawindwa ili nikamatwe. Niko tayari kukamatwa,” alisema Nkamia, ambaye anaongoza Jimbo la Chemba kwa kipindi cha pili mfululizo. 

“Nakuomba mkuu wa mkoa umuite huyu dogo (DC) umkanye kuhusu hii tabia yake ya kudhalilisha watu. Kwa kuwa bwana mkubwa (DC) hapo ameanzisha vita na sisi tunaomsaidia kazi. Sisi tuna busara zetu, hatuwezi kuingia vitani,” alisema. Nkamia alimuomba Rugimbana kuwaita wote wawili-Odunga na yeye-wakae pamoja na kutafutia suluhu ya jambo hilo ambalo alisema linaweza kukwamisha maendeleo ya jimbo hilo. Alimuonya mkuu huyo wa wilaya kuhusu tabia ya kuwatia mbaroni wananchi wanaouliza maswali wakati ni haki yao kufanya hivyo. “Chemba tulikuwa tunaishi kwa amani sana lakini amekuja bwana huyu mdogo (Odunga) anataka kutuchafulia sifa sisi. Ameteuliwa na Rais amefanyiwa vetting (uhakiki) nzuri tu. Mambo ya kuwaita watu wapumbavu no (hapana),” alisema Nkamia.

Monday, 30 January 2017

Faru Fausta wa Ngorongoro atimiza Miaka 54, Aishi Chini ya Ulinzi wa Kijeshi Saa 24

FARU Fausta ndio anayesadikiwa kuwa na umri mkubwa kuliko Faru wote duniani,mwaka huu amefikisha umri wa miaka 54. 

Faru Fausta yupo katika mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro,lakini kutokana na uzee wake huo,sasa anakabiliwa na tatizo la macho la kutoona. Kufuatia hatua hiyo,uongozi wa Ngorongoro sasa umemuweka katika makazi maalum ndani ya hifadhi hiyo. Hatua ya mamlaka kuchukua hatua ya kumpa ulinzi maalum Faru Fausta inahofia kushambuliwa na wanyama wengine wakali na hususani fisi na Simba. 

Hivi sasa gharama inayotumika kumlinda Faru Fausta ni kubwa,hivyo uongozi wa Mamlaka umeishauri wizara kuchukua hatua juu ya Faru Fausta.

Haya hapa Mambo matano kwenye Taarifa ya kwanza ya TRL kuhusu Treni iliyoanguka Ruvu

Jana January 29 2017 imetokea ajali ya Treni kwenye eneo la Ruvu ndani ya mkoa wa Pwani Tanzania ambapo Treni yenyewe inaitwa EXPRESS na ilikua ikitokea Kigoma kuelekea Dar es salaam.
Viongozi mbalimbali walielekea kwenye eneo la tukio ambapo Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Reli Tanzania (TRLMasanja Kadogosa kwenye eneo la tukio ameeleza yafuatayo.
  • Kwenye ajali iliyotokea kuna Mabehewa ambayo yametoka nje ya reli na kuanguka lakini bahati nzuri kichwa cha Treni hakikuanguka na ndio maana unaweza kuona abiria hawapo.
  • Abiria walihamishiwa kwenye Mabehewa ambayo hayakuanguka na wakaondoka na Treni hiyohiyo kuelekea Dar es salaam na nadhani wamefika kwenye mida ya saa mbili usiku, hapa kwenye eneo la tukio kuna Mabehewa ambayo yalitoka nje ya reli tu.
  • Hapa ni Kilometa 73 kutoka Dar es salaam na ni maeneo ya Ngeta Ruvu na ajali hii ilitokea kwenye saa kumi kasoro jioni, kuhusu chanzo cha ajali…. kawaida tunafanya uchunguzi na tutawapa taarifa utakapokamilika na tuna Wataalamu ndani ya kampuni ya TRL watafanya kazi yao kwenye uchunguzi.
  • Njia ya Treni imeharibika sana hapa na kuna Treni nyingine ya abiria itasafiri kutoka Dar es salaam kwenda bara kwahiyo usiku huu tutachokifanya ndani ya saa 24 tunataka tuwe tumesharudisha hii njia ili abiria na Treni nyingine za mizigo ziweze kupita na tunategemea mpaka saa tisa alasiri siku ya Jumatatu January 30 2017 Treni zipite kama kawaida.
  • Katika ajali hii tumepata Majeruhi watano na aliyeumia sana ni mmoja na alipelekwa Tumbi Hospitali iliyopo Kibaha Pwani.

Mwanafunzi Chuo cha Ardhi Dar kizimbani kwa Kuchapisha ujumbe wa Uongo Kuhusu Godbless Lema

Mwanafunzi  wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam (ARU) amefikishwa katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani akikabiliwa na kosa la kuchapisha taarifa za uongo kwenye mtandao wa What’sApp.

Akimsomea hati ya mashtaka, mshtakiwa huyo, Wakili wa Serikali, Adolf Mkini mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa alidai kuwa mshtakiwa huyo  ambaye pia anadaiwa kuwa ni kada wa Chadema Januari 3, 2017
alichapisha taarifa za uongo.

Alidai kuwa mshtakiwa huyo kupitia mtandao wa WhatsApp kwenye kundi linalotumia jina la Lowassa Foundation and Bunge Live alichapisha taarifa za uongo kuwa; Nimepata rehema ya mipango michafu sana iliyokuwa inapangwa na bado inapangwa dhidi ya uhai wa (Mb), Godbless Lema…’

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana kuhusika na kosa hilo.

Upande wa mashtaka umedai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na hana pingamizi na dhamana.

Baada ya kueleza hayo, Hakimu Mwambapa alimpa masharti ya dhamana mshtakiwa huyo ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh 2 milioni  kwa kila mmoja pamoja na barua.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo aliepuka kwenda lumande baada ya kutimiza masharti hayo ya dhamana.

Friday, 27 January 2017

Siku 118 toka aufunge uwanja wa Taifa Waziri Nape kaja na Maamuzi haya

 
Ni siku 118 zimepita toka waziri wa habari, sanaa, utamaduni na michezo Nape Moses Nnauye kutangaza kuufungia uwanja wa Taifa Dar es Salaam kutumiwa na timu za Simba na Yanga kutokana na uharibifu uliojitokeza wakati wa game yao, leo ametangaza maamuzi mapya.

Waziri Nape leo January 27 2017 kupitia wizara yake imetolewa taarifa za kuruhusu uwanja huo kuendelea kutumika kwa club zote ambapo baada ya kujiridhisha na ukarabati uliofanywa na club hizo za Simba na Yanga hivyo mechi ya Simba na Azam FC kesho itachezwa uwanja wa Taifa.

Kama utakuwa unakumbuka vizuri waziri Nape alitangaza maamuzi ya kuufungia uwanja wa Taifa Jumapili ya October 2 2016 kutokana na uharibifu na uvunjifu wa viti uliofanywa na mashabiki wakati wa mechi hiyo ikiwa ni baada ya Amissi Tambwe kuifungia Yanga goli lililotajwa kuwa la utata.

Al-Shabab Washambulia kambi ya Wanajeshi wa KENYA Nchini Somalia na Kuwaua 57

Kundi la al-Shabab nchini Somalia limesema wapiganaji wake wameshambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya wanaohudumu chini ya kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom)nchini Somalia.

Wapiganaji hao wanadai kuwaua wanajeshi wengi kwenye shambulio hilo katika kambi ya Kulbiyow kusini mwa Somalia karibu na mpaka wa nchi hiyo na Kenya.

"Mujahideen (wapiganaji) wawili walivurumisha magari yaliyokuwa na mabomu na kuyalipua kwenye lango la kambi hiyo ya mji wa Kulbiyow kabla ya wapiganaji wengine kuingia. Baada ya makabiliano makali, tumefanikiwa kuiteka kambi," mmoja wa wasemaji wa al-Shabab Sheikh Abdiasis Abu Musab ameambia shirika la habari la Reuters.

Msemaji huyo amedai kundi hilo limewaua wanajeshi zaidi ya 57 na kutwaa magari na silaha za wanajeshi hao, taarifa ambazo msemaji wa majeshi ya Kenya amekanusha.

Kanali Paul Njuguna ameambia Reuters: "Ni uongo. Operesheni ya kijeshi inaendelea. Tunaendelea kupokea taarifa."

Al-Shabab wamekuwa wakipigana dhidi ya serikali  inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi na jamii ya kimataifa.

Wanajeshi wa Kenya pamoja na wanajeshi kutoka Djibouti, Uganda na Ethiopia, chini ya Amisom, wamekuwa wakisaidia serikali hiyo yenye makao yake Mogadishu.


Januari mwaka uliopita, wapiganaji wa al-Shabab walishambulia kambi ya majeshi ya Kenya el-Adde na kuua wanajeshi wengi.

Al-Shabab walisema waliua zaidi ya wanajeshi 100. Jeshi la Kenya halijatangaza idadi kamili ya wanajeshi waliouawa hadi wa leo.
Chanzo: BBC

PICHA: Rais Barrow alivyowasili Gambia

Maelfu ya wananchi wa Gambia wamefurika katika barabara za mji mkuu wa nchi hiyo, Banjul kumlaki Rais wao, Adama Barrow wakati akiwasili nchini mwake kuiongoza nchi hiyo baada ya kuondoka madarakani kwa rais wa mda mrefu Yahya Jammeh.

Barrow aliapishwa wiki iliyopita nchini Senegal wakati viongozi walipokuwa wakimshawishi Jammeh kuondoka madarakani baada ya kushindwa katika uchaguzi uliompa ushindi Barrow.

Barrow ameamua kurudi nchini humo mapema baada ya Wanadiplomasia kumtaka arudi mara moja nyumbani kuepuka pengo la uongozi.

Kutokana na taarifa zinazoeleza kuwa wafuasi waovu wa Jammeh wamo miongoni mwa vikosi vya usalama nchini, maelfu kadhaa ya wanajeshi wa mataifa ya Afrika magharibi wanasalia Gambia ili kuimarisha ulinzi kwa Rais Barrow.

Barrow atakaa katika makazi yake wakati ukaguzi ukifanywa katika Ikulu kutambua hatari yoyote kufuatia kuondoka kwa Yahya Jammeh kwenda uhamishoni Guinea ya Ikweta.
 
Maelfu ya wananchi wa Gambia waliojitokeza kumlaki Rais wao
 

Watu 14 akiwemo raia wa China wahofiwa kufa Mgodini

Watu 14 akiwemo Mchina, wanahofiwa kufa baada ya kufukiwa katika mgodi wa dhahabu wa Kampuni ya RZ Union Mining Ltd uliopo Kata ya Nyarugusu mkoani Geita.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Ezekiel Kyunga jana alisema watu hao wamefukiwa chini ya mgodi baada ya mlango wa kuingilia kwenye shimo la mgodi kumeguka udongo na kujiziba.

“Usiku wa kuamkia leo (jana) saa tisa kwenye mgodi huo unaoendeshwa na Wachina, mlango wa kuingilia mgodini mmoja ulimeguka na kujifunga watu 14 wakiwa ndani,” alisema Kyunga.

Kyunga alisema kwa mujibu wa kitabu cha orodha ya watu wanaojiandikisha kuingia mgodini, kuna majina ya Watanzania 12 na Mchina.

Aidha, alisema mbali na watu hao 13, pia kuna Mtanzania mmoja ambaye aliingia bila kujiandikisha na hiyo ni kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo hivyo kufanya idadi ya watu waliofukiwa kuwa 14. 

Kyunga alisema tangu jana asubuhi jitihada mbalimbali za kuondoa udongo kuwaokoa watu hao zinaendelea wakitumia mitambo na wataalamu.

“Kwa kusaidiana na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) na wataalamu wengine, jitihada zinaendelea ili kuhakikisha tunawaokoa watu hao,” alisema Kyunga. 

Alisema wakati huo huo wamefanikiwa kutoboa eneo jingine na kupitisha mabomba ya hewa ya oksijeni ili kuwafanya watu hao wasikose hewa.

Thursday, 26 January 2017

Tetesi Kuhusu Adebayor kutua Yanga,..isome hii ya BBC SPORTS kwa makini


Jana January 25 2017 moja kati ya taarifa zilizokuwa zimeenea katika mitandao ya kijamii ni kuhusiana na mshambuliaji wa kimataifa wa Togo aliyewahi kucheza ArsenalMan CityTottenham Hotspurs na Crystal Palace  Emmanuel Adebayor kuripotiwa kujiunga na  timu ya Yanga.
Habari kutoka soka25east.com na mitandao mingine mitatu ya Kenya zilisema kuwa staa huyo atajiunga na Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania bara Yanga ambayo pia inachezewa na Vincent Bossou anayechezea timu moja ya taifa na Adebayor na walikuwa pamoja AFCON juzi.
Saa 24 baada ya taarifa hizo kupita mitandao ya Skysports na BBC SPORTS imeripoti na kumnukuu Adebayor kuhusu mpango wake wa sasa katika soka akiwa mchezaji huru, anasema bado ana mpango wa kurejea ligi kuu England na hajaizungumzia Yanga hata tone, hiyo imedhihirisha kuwa tetesi za kujiunga na Yanga sio za kweli.

Nimepokea ofa chache kutoka timu za ligi kuu England na wote mnajua napenda kucheza England, licha ya kuwa mimi sio moja kati ya wachezaji wanaopendwa England nimecheza England kwa miaka kumi, ieleweke pia sikuja AFCON kucheza ili nipate timu nilikuja kuwakilisha taifa langu

Faini yamgeukia Trafiki Dar es Salaam, aagizwa na Boss wake kulipa yeye badala ya mwenye Benz

Jana January 25 2017 kuna comment ambayo ilikua inasambaa sana kwenye Whatsapp ikionyesha post ya Facebook ya Mtanzania ambaye amepigwa faini na Askari wa usalama barabarani (Trafiki) kwa kosa la Ubovu wa gari lake.
Post yenyewe ya Mlalamikaji akiwa kaambatanisha picha za sehemu ya gari yenye kutu ilisema ‘Jamani nimepigwa cheti at gari ni mbovu, hii kweli ni sahihi?
Pamoja na hiyo post kuna Comment ya Facebook ikionyesha account yenye jina la Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mohammed Mpinga ikiwa imetoa comment kwa kusema ‘nimefuatilia leo asubuhi TAZARA na kubaini kwamba hakustahili kosa la ubovu wa rangi au kutu inayoonekana, nimeelekeza askari huyo alipe mwenyewe hiyo faini na kupewa onyo kali
Wengi wanataka kujua kama ni kweli hiyo Account ya Facebook ni ya Kamanda Mpinga? na ni kweli alijibu hivyo? ni baadhi ya maswali watu waliyonayo ambapo  Kamanda Mpinga amesema ‘Hiyo ilikua ni kweli, account na Facebook comment ni mimi nimetoa

Trump Kaanza Kuwatimua Watu Marekani.......Tayari Wasomali 90 na Wakenya 2 wameondolewa Marekani

Raia takriban 90 wa Somalia na wawili wa Kenya wametimuliwa kutoka Marekani saa chache baada ya taarifa kuibuka kwamba Rais Donald Trump atakabiliana na watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.

Wote wamewasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi.

Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe ameambia BBC kwamba raia hao wa Somalia watasafirishwa moja kwa moja hadi Mogadishu.

Bw Trump alisema Jumatano itakuwa siku muhimu kwa usalama wa Marekani.

Anatarajiwa kuweka masharti makali kwa raia wa mataifa saba ya Mashariki ya Kati na Afrika yenye idadi kubwa ya Waislamu wanaotafuta viza za kwenda Marekani.

Nchi hizo ni Syria, Iraq, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen

Wednesday, 25 January 2017

Trump Kuzuia wahamiaji kutoka nchi za Kiislamu Afrika na Mashariki ya Kati........Pia Ataweka Sheria Kali ya Kupata Visa

Rais wa Marekani Donald Trump anatarajiwa kutia saini sheria  kuweka masharti kuhusu wahamiaji wanaoingia nchini humo.

Taarifa kutoka Marekani zinasema ataanza kwa hatua ya kuimarisha usalama katika mpaka wa nchi hiyo na Mexico atakapozuru makao makuu ya wizara ya usalama wa ndani leo  Jumatano.

Aidha, anatarajiwa pia kutoa tangazo la kuidhinisha sheria kali zaidi za kupata visa kwa wageni kutoka eneo la Mashariki ya Kati na Afrika ambayo yana Waislamu wengi

Bw Trump ameandika kwenye Twitter kwamba leo itakuwa siku muhimu sana kwa usalama wa taifa la Marekani.

Wakati wa kampeni yake ya urais, Donald Trump aliahidi kufanyia mageuzi suala la uhamiaji Marekani.

Aligusia ujenzi wa ukuta kati ya Mexico na Marekani kuzuia wahamiaji haramu na kuwapiga marufuku Waislamu kuingia katika taifa hilo kama sehemu ya vita dhidi ya ugaidi. 
Baadaye alibadili msimamo kidogo na kufafanua kwamba watakachofanyiwa Waislamu ni kufanyiwa ukaguzi mkali kabla ya kuruhusiwa kuingia Marekani.

Anatarajiwa kufika katika wizara ya usalama wa ndani baadaye leo na anatarajiwa kusaini maagizo hayo ya kuimarisha usalama katika mpaka wa Mexico na taifa lake na baadaye wiki hiii taarifa zinaashiria atawajibikia ahadi yake ya kupunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Marekani.

Na hiyo ni hadi pale ukaguzi mkali utakapoanzishwa na kuzuia raia wa mataifa saba ya Afrika na kutoka eneo la Mashariki ya Kati yote yalio na idadi kubwa ya waumini wa Kiislamu.

Ubaguzi wa kidini unapigwa marufuku kwa mujibu wa katiba ya Marekani lakini inadhaniwa utawala wa Trump utaidhinisha marufuku hiyo kwa misingi kwamba ni hatua za dharura kukabiliana na tishio lililopo la ugaidi.

Awali, Bw Trump aliandika kwenye Twitter kueleza kusikitishwa kwake na kiwango cha juu cha ghasia na mauaji katika jiji la Chicago.

Vyombo vya habari wiki hii viliripoti kwamba tayari watu 228 wamepigwa risasi na wengine zaidi ya 40 kuuawa mwaka huu.

Bw Trump ameandika kwamba iwapo watawala wa Chicago hawatatatua tatizo hilo la mauaji, basi atawatuma 'Feds' akimaanisha maafisa wa FBI.
Chanzo: BBC

Tuesday, 24 January 2017

Kauli ya Tundu Lissu baada ya chaguzi ndogo kumalizika na CCM kuibuka kidedea

Na. Tundu Lissu 
Waheshimiwa na makamanda poleni kwa mapambano na hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya kwenye chaguzi hizi. Naona kila mmoja wetu anasikitika jinsi matokeo ambavyo yamekuwa tofauti na matarajio yetu na kazi tuliyoifanya.


Ni rahisi, katika mazingira haya ya kushindwa na kabla vumbi halijaisha, kuanza kulalamika, kunyoosheana vidole na kukatishana tamaa. Hii haitusaidii sana. Badala yake, tunachohitaji zaidi ni ‘brainstorming’ kuliko ‘blamestorming.’ Naomba nifanye ya kwanza. Chaguzi ndogo za ubunge au udiwani ni ngumu sana kushinda katika mazingira halisi ya nchi yetu.

Mifano michache inathibitisha ukweli huu. Katika election cycle ya ’05-’10, tulishinda Jimbo la Tarime lakini tukapigwa Biharamulo Magharibi na Busanda. Tarime lilikuwa Jimbo letu tangu Uchaguzi Mkuu wa ’05, Busanda lilikuwa la maCCM na Biharamulo Magharibi lilikuwa la TLP. Sikumbuki vizuri kama tulishinda Kata hata moja katika mzunguko wa uchaguzi wa kipindi hicho.

Katika election cycle ya ’10-’15, tulipigwa Igunga licha ya kazi kubwa tuliyofanya, lakini tukashinda Arumeru Mashariki iliyokuwa chini ya maCCM. Vile vile tulishindwa Kalenga, Chalinze na Ulanga Magharibi yaliyokuwa ya maCCM tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.

Kwenye chaguzi za Kata za ’12 kama mnakumbuka, licha ya kazi kubwa na rasilimali nyingi, tulipata Kata tatu tu kati ya 26 zilizokuwa zinagombaniwa. Ukiachia Ifakara Mjini ya Mh. Juakali, Kata nyingine mbili – Kiboriloni na Iseke – zilikuwa zetu tangu Uchaguzi Mkuu wa ’10.

Kwa mantiki hii, matokeo ya jana sio ya kushangaza sana. Kata ya Duru ilikuwa ya kwetu na tumeitetea, nyingine zote tulikopigwa zilikuwa za maCCM. Hatujanyang’anywa iliyokuwa yetu, hatujanyakua zilizokuwa zao. Hata hivyo, funzo kubwa zaidi la historia ya chaguzi hizi ni hili hapa: licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo hizi, tumeendelea kufanya vizuri zaidi katika kila Uchaguzi Mkuu uliofuatia kipigo cha chaguzi ndogo.

Mwaka ’10 tulifanya vizuri zaidi licha ya kupigwa Busanda na Biharamulo Magharibi katika mzunguko wa ’05-’10. In fact, tulichukua Jimbo la Biharamulo Magharibi mwaka huo. Na tulipata Kata nyingi zaidi ’10 kuliko ilivyokuwa ’05. Mwaka ’15 tulipata ushindi mkubwa zaidi katika Kata na majimbo licha ya kupigwa kwenye chaguzi ndogo za mzunguko wa ’10-’15.

Hoja yangu hapa ni kwamba uchaguzi wa marudio hauna direct and negative bearing kwenye matokeo yetu ya Uchaguzi Mkuu unaofuatia. On the contrary, uchaguzi wa marudio unatupa fursa ya kupanda mbegu ambayo, ikitunzwa vizuri, inakuwa na mazao bora kwenye chaguzi zinazofuatia.

Kwa upande mwingine, chaguzi za marudio – kwa sababu ya udogo au uchache wa maeneo yanayogombaniwa – yanawapa maCCM fursa ya kutumia nguvu kubwa za rasilimali na za kidola ukilinganisha na tunazotumia sisi. Kwenye Uchaguzi Mkuu unaofuatia, nguvu hizo zinasambazwa nchi nzima na kwa hiyo effectiveness yake inapungua.

Ndio maana tumefanya vizuri zaidi kwenye Uchaguzi Mkuu kuliko kwenye chaguzi ndogo za marudio. Hili, kwa maoni yangu, ndilo fundisho kuu la chaguzi hizi za marudio. Hatuna sababu kubwa ya kushangilia kutokana na matokeo ya jana. Hata hivyo, hatuna sababu yoyote ya kuomboleza pia. Obviously, maCCM na wapambe wao wataandika ‘wasifu wa marehemu’ wa CHADEMA/UKAWA na kuutangaza dunia nzima na kwa sauti kubwa. Hilo lisitupofushe macho yetu, hata kama linakera sana.

Tutathmini kazi tuliyoifanya na matokeo tuliyoyapata. Tupate mafundisho sahihi ya kazi hiyo na matokeo yake. Tutumie mafundisho hayo kwa kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya ‘the real prize’: 2020.

Donald Trump kawafuta kazi Mabalozi wote wa Marekani duniani

Kwa mujibu wa The Independent na ParsToday wanasema kuwa Rais Donald Trump wa Marekani amewafuta kazi mabalozi wote wa nchi hiyo kote duniani na wanaohudumu katika mashirika ya kimataifa ambapo uamuzi huo umefanyika katika siku yake ya kwanza kazini.
 
Trump ambaye aliapishwa Ijumaa January 20, 2017 kuwa Rais wa 45 wa Marekani, amewataka mabalozi wote walioteuliwa na mtangulizi wake, Barack Obama kuondoka kazini mara moja bila hata kuwapa muda wa kujitayarisha kuondoka kama ilivyo kawaida.
 
Inaelezwa kuwa zaidi ya mabalozi 80 wa Marekani katika nchi mbalimbali duniani walifutwa kazi Ijumaa tarehe 20 Disemba saa sita mchana ikiwa ni mara baada ya Trump kuapishwa.
 
Hatua hiyo ya Trump inatazamiwa kuvuruga uhusiano na washirika muhimu kama vile Ujerumani, Uingereza na Canada ambapo ripoti zinasema nchi hizo zinaweza kukaa bila mabalozi kwa miezi kadhaa kwani baada ya Trump kuteua mabalozi wapya watalazimika kuidhinishwa na Bunge la Congress kabla ya kuanza kazi zao.
 
Donald Trump anakosolewa kwa kuacha nafasi nyingi wazi na hivyo kuvuruga shughuli za kawaida za serikali ya Marekani na hii haya yanajiri huku maandamano yakiripotiwa kuendelea sehemu   mbalimbali kupinga utawala wa kiongozi huyo.
 
Nchini Marekani katika siku ya pili ya utawala wa Trump kumeripotiwa maandamano ya watu milioni tatu na imeripotiwa kumefanyika maandamano 637 katika maeneo mbalimbali ya Ulaya, Asia na Afrika kumpinga rais mpya wa Marekani.

Monday, 23 January 2017

Waziri Anjela Kairuki aiaga Dar leo na Kuhamia Dodoma

Waziri wa utumishi wa umma na utawala bora Angela Kairuki leo January 23 2017 ameiaga rasmi Dar es salaam na sasa ofisi za Wizara hiyo zinahamia Dodoma katika ofisi mpya ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais, agizo ambalo linawataka ifikapo February 28 2017 ofisi za serikali ziwe zimehamia Dodoma.

Nje ya Wizara hiyo Wafanyakazi walionekana wakipunga mikono kwa ishara ya kuaga ambapo Malori ya Jeshi ndio yanayotumika kuhamisha mizigo ambapo Waziri Angela Kairuki ameeleza kuwa vifaa hivyo ni vya kundi la kwanza linalohusisha Uongozi wa juu wa Wizara.

Vifaa hivyo vya ofisi vilivyosafirishwa kwa awamu ya kwanza ni vya Waziri wa nchi ofisi ya Rais, menejimenti ya utumishi wa umma na utawala bora, katibu mkuu na naibu katibu mkuu na baadhi ya wakurugenzi, wakurugenzi wasaidizi, maafisa waandamizina watumishi wengine na kwamba jumla ya watumishi 87 watahamia
Dodoma katika awamu hii ya kwanza

Malori ya Jeshi yakiwa yamebeba mizigo tayari kwa safari ya Dodoma

PICHA: Magari ya Kifahari ya Rais Jammeh Yaliyozuiliwa Uwanja wa Ndege Likiwemo Lenye Thamani ya Zaidi ya Tsh. Milioni 500

Yahya Jammeh aliyeitawala Gambia kwa miaka 22, hatimaye jana aliondoka nchini humo na kwenda kuishi uhamishoni baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Disemba Mosi mwaka jana.
Jammeh alishindwa na kiongozi aliyekuwa akiungwa mkono na vyama vya upinzani, Adama Barrow ambaye amekuwa akiishi nchni Senegal alipoapishwa kuwa Rais wa Gambia baada ya Jammeh kukataa kutoka madarakani awali.

Yahya Jammeh alipokuwa akiiongoza Gambia aliweza kujinunulia vitu vingi vya kifahari na moja wapo ni gari lake la kifahari aina ya Rolls Royce.

Gari hili ambalo kwenye viti vyake ameandika jina lake, lina thamani ya kati ya fedha za kitanzania milioni 500 hadi milioni 800. Rolls Royce ni moja ya magari ya kifahari na ya kipekee duniani ambayo mara nyingi hutumiwa na watu wenye uwezo mkubwa kifedha.

Gari hili la Yahya Jammeh liliwashangaza raia wengi wa Gambia lilipokuwa likikatisha katika viunga vya mji wa Banjul kumpeleka kiongozi huyo uwanja wa ndege tayari kuondoka nchini humo.

Licha ya kuwa Jammeh aliondoka nchini Gambia jana huku wananchi wakishangilia kwa furaha, imeelezwa kuwa kiongozi huyo alikomba fedha katika hazina ya nchi hiyo na kuiacha katika ukata mkubwa wa fedha.

Taarifa kutoka katika kambi ya Rais Adama Barrow zinaeleza kuwa dola za kimarekani milioni 11 zilichukuliwa katika hazina ya nchi hiyo.

Yahya Jammeh tayari amewasili nchini Equatorial Guinea ambapo ndipo ataishi.


Hapa chini ni picha zaidi za gari hilo la kifahari;
 
 
 
Hapa ni sehemu ya magari ya Yahya Jammeh yaliyopo uwanja wa ndege wa Banjul Gambia, baada ya ndege toka Guinea kuzuiliwa kuyachukua.  
 

Profesa Lipumba Anusurika Kipigo kutoka kwa Vijana wa UKAWA

Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amenusurika kupigwa na vijana wanaoaminika kuwa ni wa Ukawa wakati akitoka kwenye mkutano wa kampeni mjini Morogoro.

Katika vurugu zilizotokea juzi jioni wakati vijana wa Ukawa na kikundi cha ulinzi cha CUF (blue guard) cha Dar es Salaam wakiwa na Profesa  Lipumba walikuwa wakitoka kwenye mikutano ya kampeni maeneo tofauti walipokutana barabarani na kuanza kurushiana maneno na hatimaye kupigana.

Katika vurugu hizo, vijana wa Ukawa waliwazidi wenzao wa blue guard na Profesa Lipumba kulazimika kukimbilia kwenye Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja ili kujinusuru.

Ghasia hizo zilidumu kwa takribani saa moja na nusu ambapo baada ya Profesa Lipumba kukimbilia msikitini hapo, wafuasi wa Ukawa walibaki nje mpaka polisi walipofika na kuwatawanya.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonce Rwegasira alikiri kutokea kwa vurugu hizo ambapo alisema wafuasi watatu wa CUF walijeruhiwa.

Alisema kuwa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini walioanzisha vurugu hizo ikiwa ni pamoja na kuweka doria kali katika mikutano ya vyama vya siasa.

Profesa Lipumba hakupatikana jana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake kutokuwa hewani jana

Friday, 20 January 2017

Maiti iliyozikwa na Baadae Kukutwa Iko Nyumbani Kitandani Yazikwa Tena Chini Ya Ulinzi Mkali wa Polisi

Maiti ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.

Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.

Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) na mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini Mbeya.

Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.

Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.

Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza kaburi lifukuliwe.

Lakini juzi baada ya kukamilishwa kwa taratibu husika, ikiwemo kupatikana kwa kibali kutoka mahakamani, saa nne na nusu asubuhi, Polisi Mkoa wa Mbeya walifika eneo la makaburi alipozikwa marehemu na kusimamia shughuli nzima ya kufukua kaburi hilo.

Shughuli hiyo iliyodumu kwa muda wa nusu saa kama ilivyokuwa siku ya kwanza, ilihudhuriwa na mamia ya wakazi jijini hapa waliotaka kujua nini kilichozikwa ilhali mwili ukiwa umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa wakati huo.

Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.

Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea na taratibu za maziko kwa mara nyingine.

Baada ya ndugu kukabidhiwa mwili, jeshi hilo pia lilisimamia maziko yaliyofanyika upya saa 10 jioni katika kaburi lile lile la awali, lakini tofauti na awali, kabla ya kuzika ulifanyika utaratibu wa ndugu, jamaa na marafiki waliohudhuria, kuuaga mwili wa marehemu uliokuwa ndani ya jeneza lililofunuliwa upande wa kichwani.

Kutokana na mkanganyiko uliojitokeza, baadhi ya ndugu na majirani wa Mtaa wa Igoma, walisema tukio hilo linaweza kuwa na sura mbili kwa maana ya hujuma iliyofanywa kwa makusudi, ikilenga maslahi binafsi ya mtu inayohusishwa na imani za kishirikina au bahati mbaya ya kuusahau mwili wa marehemu.

Walisema inaweza kuwa hujuma kutokana na kawaida ya misiba kabla ya maziko, lazima ndugu watoe heshima za mwisho kwa marehemu, lakini kwa msiba huu haikufanyika pamoja na baadhi ya ndugu kutohudhuria mazishi.

Akizungumza  nyumbani kwake jana pamoja na kukanusha tuhuma za kuhusisha tukio hilo na imani za kishirikina, baba wa marehemu alisema mkanganyiko uliojitokeza wakati taratibu za kuuandaa mwili zikifanyika pamoja na uzushi uliofanywa na mchungaji, ambaye alisema hamjui kwa jina, ndiyo vilivyokuza jambo hilo.

Alisema kama ilivyo kawaida baada ya majirani kupata taarifa za msiba wakiwa nyumbani hapo, walichanga fedha na kutuma watu kwenda kununua jeneza.

“Wananchi walichanga hela wakanunua jeneza likaletwa nyumbani. Waliobeba jeneza walilisukumiza tu kwenye chumba wakatoka, sisi tukaendelea na taratibu nyingine za mazishi. Baadaye akaja mwenyekiti akasema toeni mwili wa marehemu nje, wakatoa meza nje wakatuma vijana waende kuchukua mwili wa marehemu ndani. Waliopeleka jeneza ndani na waliokwenda kulichukua ni watu wengine. Jeneza likawekwa juu ya meza tukaendelea na mahubiri,” alisema Kyando.

Alisema baadaye walikwenda kuzika na baada ya kuzika walirudi nyumbani kisha wakala chakula na kunawa maji, kama ilivyo desturi ya misiba mingi mkoani hapa.

“Tumenawa maji tukakaa. Baada ya kukaa kuna mgeni akaingia katika chumba tunacholala ambapo awali ndipo tulimlaza mtoto kwenye kigodoro, alipoweka begi akakuta kuna blanketi. 

"Alipolifunua akashtuka akasema kuna nyoka watu wakaanza kukimbia ndani. Baadhi ya watu wenye roho yenye hasira wakaamua kuingia ndani wakahakikishe kuna nini,” alisimulia. 

“Walipoingia ndani ndipo wakakuta ni mwili wa mtoto yaani marehemu. Waliposema ni mtoto wakipaza sauti watu wakajaa ndani. Ndipo waumini wa yule mchungaji wakaanza kumpigia simu yule mchungaji baadaye akarudi.”

Alisema baada ya mchungaji huyo kufika, aliingia ndani na waumini wake na kuanza kuomba.

“Walipoomba kwa muda mrefu ndipo mchungaji huyo alipotoka nje na kushika MIC na kuuambia umati kuwa mtoto baada ya kuombewa amehema mara mbili na ndipo watu wakaanza kulumbana,” alieleza.

“Kama siyo mchungaji kuzusha yale wala yasingekuzwa mpaka kwenye mitandao kiasi hiki. Sisi tunaamini walioagizwa kuchukua mwili walichukua jeneza tupu pasipo kuwekwa mwili ndani yake na kwa kuwa baada ya kutolewa jeneza hatukuingia ndani hivyo tuliuacha mwili nyumbani tukaenda kuzika jeneza peke yake,” alibainisha.

Akizungumzia suala la imani ya familia hiyo, Kyando alisema awali yeye na familia yake yenye watoto wawili, walikuwa wakisali katika Kanisa Katoliki, lakini kutokana na matatizo ya degedege yaliyokuwa yakimsumbua mwanawe wa kwanza, mkewe aliamua kumpeleka mtoto huyo kwa mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe ikiwa ni sehemu ya kuhangaikia afya ya mtoto.

“Tulikuwa tunasali Roma, lakini kutokana na matatizo ya mtoto, mama yake akaamua aanze kusali Kanisa la Bonde la Baraka ili aombewe. Hapo mimi nikaacha kusali na ndiyo sababu hata katika ibada ya maziko ya mtoto ikabidi tulishirikishe kanisa walikokuwa wanasali mama na mtoto,” alisema Kyando na kuongeza: 

“Watu wamezungumza maneno mengi sana, siwezi kubisha japo ni ya uzushi ila wameongea kutokana na walivyosikia, ila ukweli naujua mimi na namwachia Mungu.”

Naye baba mkubwa wa marehemu, Saulo Kyando alisema jambo lililotokea lilikuwa la kawaida na kilichotokea ni kukosekana kwa uratibu makini wa msiba huo.

“Hili jambo lilikuwa la kawaida sema kilichokosekana ni mtu ambaye angeliweka jambo sawa, angekuwepo mtu wa kusimamia kila hatua yasingefikia hapa,” alisema Saulo.
 Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma pamoja na Baba wa Marehemu wakifunua jeneza kuhakikisha kama kulikuwa na mwili wa marehemu 
 Jeneza baada ya kufukuliwa kutoka kaburini
Vijana wakiwa wanaondoa jeneza makaburini na kulipeleka kituo cha Polisi kwa ajili ya taratibu zingine.

Blog Archive