Kama unakumbuka December 10 2016 Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa aliunda tume baada ya kupokea pembe mbili za
faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika kumhamisha faru huyo.
Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa December 6, 2016, akiwa ziarani
mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika
kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
March 27 2017 Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amepokea
taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo cha Faru John
kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele ambaye alikuwa
akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri
Mkuu, Prof. Manyele amesema tume yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha
Faru John kwa kupima vinasaba vya sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga,
fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na kinyesi kilichokaushwa ambapo
ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja, aina ya faru mweusi ambaye ni
dume.
Prof. Manyele amesema matokeo hayo
yamethibitisha kuwa faru John alikufa katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti
kwa kukosa matunzo na uangalizi wa karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo
Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini ya usimamizi wa timu ya
wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa Serikali, chini ya Ofisi ya
Mkemia Mkuu wa Serikali. Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa
matunzo na uangalizi wa karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea
yanayotokana na kutofuata taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya
kiuongozu kwa Wizara husika, hifadhi na taasisi zake,”
Prof. Manyele amesema mapungufu
waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo ni kutokuwepo kwa kibali rasmi
cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa mkataba wa kupokelewa kwa Faru
John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo
ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli
za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi;
migongano ya kimaslahi kati ya watumishi waliolenga kusimamia taratibu
na wale wenye kusimamia maslahi binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye
mamlaka sawa juu ya masuala ya uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na kwamba mawasiliano
yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi
kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori cha kuruhusu kumhamisha Faru John
kutoka NCAA kwenda Grumeti,” Prof. Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia kuhusu uchukuaji holela wa
sampuli za wanyama pori kwa lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya
nchi, Prof. Manyele amesema kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli
wanazochukua haziwekwi vizuri na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA
wapewe msisitizo juu ya umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kusomewa ripoti huyo, Waziri Mkuu aliishukuru timu ya
uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa kazi
iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo ndani ya Wizara ya
Maliasili na Utalii na taasisi zake.
“Ofisi yangu itaipitia taarifa
hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia kazi. Matokeo ya kazi hiyo,
tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha Serikali imeamua kufanya nini juu
ya mapendekezo yaliyotolewa.”
www.domdaily14.blogspot.com
Tuesday, 28 March 2017
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment
Toa Maoni Yako Hapa (Zingatia Maadili)